MWANDISHI: EMMANUEL MBOGO
WACHAPISHAJI: HEKO PUBLISHERS
MWAKA: 2002
JINA LA KITABU
Jina la kitabu WATOTO WA MAMA NTILIE limesadifu yaliyomo ndani ya kitabu, kinaeleza kuhusu maisha ya watoto wa mama ntilie. Maisha ya dhiki, umaskini uliokithiri, maisha yasiyo ya faraja yaliyokosa malezi bora, chakula bora, elimu, huduma ya afya nk. Jina la kitabu linaakisi yaliyomo ndani ya kitabu na katika jamii yetu ya leo kwani akina mama wengi hawana kazi nzuri za kuwaingizia kipato kikubwa na bado wanategemewa katika malezi. Mwandishi ametumia jina hili ili kibua kero na matatizo yaliyoko katika jamii.
UTANGULIZI WA KITABU
Riwaya ya Watoto wa Mama N’tilie ni riwaya ambayo inasadifu maisha ya Mtanzania wa leo. Inaangazia suala la umaskini na hali ngumu ya maisha, wimbi la watoto wa mitaani, masuala ya uhalifu wizi na ujambazi, malezi nk. Mwandishi Mbogo amejitahidi sana. Pia katika fani ametumia muundo na mtindo wenye kuwavutia wasomaji pia kawaumba wahusika wake kwa usadifu wa hali ya juu huku mandhari yake ikiwa ni halisi inayosawiri maisha ya Tanzania.
MUUNDO
Muundo uliotawala katika riwaya hii ni muundo wa rukia au rejea. Mfano sura ya tatu mwandishi anatuelezea juu ya safari ya Mama ntilie kwenda matombo uk.34. Lakini anaacha kisa hicho ndani ya sura hiyohiyo anaanza kutuelezea juu ya kuzaliwa kwa watoto Kurwa na Doto na asili yao. Pia uk.80 mwandishi anatudokeza juu ya safari ya kwenda kwa Musa na hatuoneshi hatma ya safari yake bali anarukia kisa kingine na kuanza kutuelezea juu ya Zita kupandwa na kichaa uk.81. Vilevile uk.85-86 anatusimulia juu ya safari ya Mama Zita na Zenabu kuelekea hospitali kumwona Zita lakini hatuoneshi hatma ya safari yao bali anarukia kisa kingine na kuturudisha nyumbani kwa Mzee Lomolomo na jinsi anavyofakamia pombe alafu anaturudisha tena kutuambia juu ya kifo cha Zita hospitalini Muhimbili.
Mwandishi amegawa visa na matukio katika sura tano. Sura hizi zimejengwa katika muundo unaotegemeana ili kukamilisha kilele cha masimulizi.
MTINDO
Mtindo aliotumia mwandishi ni wa masimulizi ya mjazo au lugha ya nathari ameeleza visa mwenyewe na vingine wahusika wamevielezea. Pia ametumia mitindo kadha wa kadha. Mfano;
Nafsi ya tatu wingi na umoja
Uk.15 “Peter aliokota kipande cha muhogo” “alisafisha kipande cha muhogo”
Uk.27 “walisaidiana wakaubeba” uk.26 “watu walisongamana walisukumana…..”.
Kwa kiasi kikubwa matumizi ya nafsi ya tatu ndiyo yaliyotawala.
Nafsi ya kwanza umoja na wingi
Uk.58 “nitasema nitasema!”
Uk.58 “njoo tuongee”
Uk.56 “twende tule”
Matumizi ya nafsi ya pili au dayalojia
Uk.89 pale Mama ntilie alipokumbuka majibizano yake na Zita.
MAMA NTILIE: na hiyo nguo namna gani? Mbona chafu hivyo na leo ndio kwanza
Jumanne.
PETER: mbwa Mama……
ZITA: amenikwaruza kidogo na makucha yake.
Matumizi ya tanzu nyingine za kifasihi, mfano wimbo
Uk.78 “Jua ni moto
Tena ni mwangaza
Wa Dunia
Nadina yoo
Nadina mama
Tumwombe Mungu Baba”
Uk.10 wimbo alouimba mzee Lomolomo.
“Kuleni nae
Hata bangi vuteni nae
Lakini ni kazi bure
Mwenzenu nimezaa naye
Pepepe kijani cha mbaazi
Kijaluba na msondo
Kiboko yao”.
Hivyo mwandishi ametumia mitindo hiyo ili kutomchosha msomaji mfano wimbo unamburudisha msomaji, majibizano yanavuta umakini zaidi na matumizi ya nafsi mbalimbali.
MATUMIZI YA LUGHA
Riwaya ya Watoto wa Mama Ntilie imetumia lugha rahisi, fasaha na inayoeleweka kwa wasomaji. Kuna matumizi ya lugha ya kiingereza mfano. Uk.36 “chloroquine”, “Rosewine na Queen Elizabeth”, Uk.83 “faster faster mama” uk.1 “landrover”. Pia kuna matumizi ya lugha ya miitaani uk.41 “kudeku…..”
Tashibiha
uk.10 “mdomo wake ulio kaa kama bakuli la pombe”
Uk.12 “mama ntilie alikaa kama kapigwa na radi”
Uk.15 “miguu kama ya mamba”
Uk.46 “aliinamisha shingo nayo ikapinda kama mforosadi” “kichwa kama stafeli”
Uk.40. “kitovu chake kama jicho chongo”
Uk.23 “Kurwa aliruka nyuma kama Chui”
Uk.45 “akaruka kama Paa”
Tashihisi
Uk. 10 “mabega yenyewe tayari yalikuwa yamechongwa kwa pombe ya gongo
Yameangalia juu karibu yakutane na masikio”
Uk.17 “aliziona nywele za kipilipili za Musa ngumu kama katani hazijaonja maji wala
sabuni”
Uk.19 “ moshi wenye harufu ya kuudhi ulilelea hewani na kumlaki mtoto Peter.”
Uk.35 “…… visogo vitatu vilikata kona na kupotea”
Uk.46 “koo lilimsaliti”
Uk.40 “miguuni raba zinazocheka kwa huzuni”
Uk.46 “mlango ule wa kuungwa na gundi ulitika labeka”
Sitiari
Uk.10 “Nyama nyie”
Uk.86 “…… wakatembea mwendo wa Farasi”
Ritifaa
Uk.38 “Mama? Mama yuko wapi, Baba yuko wapi? Mapenzi yao yako wapi?”
Uk.92 “Zita! Zita! Zita! Zita umekwenda! Umenitoroka, Zita mwanangu”
Uk.93 “Baba! Baba watoto? Mwenzangu! Ee! Amka, simama! Usiniachie tanzia hii peke
Yangu”
Tafsida
Uk.91 “haja kubwa”
Onomatopea /tanakali sauti
Uk.5 “….. aliupinda mgongo kwa mbele akausikia unalia ka-ka-ka-ka, alitema mate tena
Phuuuu”
Uk.11 “alikohoa ukho! okho!”
Uk.19 “…. Kwa kupiga chafya mbili au tatu Tcha! Tcha! Tcha!”
Uk.50 “Bwee! Bwee! Bwee! Mbwa ….”
Uk.50 “Hali … vicheko Woo! Woo! Weee! Weee! Heheheee! Leooo!”
Takriri
Uk.12 “twende! Twende! Nakuwacha nakauwacha!”
Uk.58 “ Nivione! Nivione! Nivione vya kazi gani!”
Uk.60 “ Nipishe! Nipishe! Nipishe!
Uk.61 “kukurukakara, kukurukakara,kukurkakara”
Uk.91 “ Baba! Baba! amka Baba”
Mjalizo
Uk. 40 “… akapata pesa, akala, akashiba”
Mdokezo
Uk.58 “usiseme hivyo! Unasikia ee! Usi……”
Uk.71 mara akaanza kuimba tena uleule wimbo wake wa “siwezi kuuwa mtu
mama”
Uk.73 “lakini…….”
Uk.79 “ alikumbuka jaa laa jiji na ………”
Nidaa
Uk.44 “ Oh! Mungu wangu!”
Uk.91 “ Mama wee!”
Uk.90 “Hamadi! Mtume!”
Nahau
Uk.43 “…. Kupiga usingizi”
Methali
Uk.34 “ kamba hukatikia pembamba”
Uk. 69 “fadhila za Punda”
Misemo
Uk.35 “ mtu wa maji” – mlevi.
Uk.13 “kwake pombe ya mataputapu na gongo alivifanya dini”.
Taswira mwonekano mfano
Uk.1 “ Mbwa huyu mweusi mwenye mkia mweupe, alionekana akitembea mwendo wa polepole. Ulimi wake mrefu ulionekana ukidondoka mate ya utelezi” hii inatufanya tupate picha halisi ya jinsi Mbwa huyo alivyo kupitia maneno ya msanii”.
Uk.5 “….. hatua tatu mbele yake Sufuria, Vikombe na Sahani chafu zilizagaa pale nje zikimtazama. Akawaona nzi wakitembea na kurukaruka juu ya vyombo vichafu.
Uk.10 “ mabega yenyewe tayari yalikuwa yamechonngoka kwa pombe ya gongo yameangalia juu karibu yakutane na masikio.”
Uk.69 “Zenabu alibaki pale mlangoni kavaa gauni aina ya shifti, kitambaa cha Hariri”
Taswira hisi
Uk.91 “ Mzee Lomolomo alilala mdomo wazi Nzi wakubwa wa kijani kibichi wamejaa tele mdomoni mwake”. Hii inamfanya msomaji ajisikie kinyaa kutokana na hali hiyo ya Mzee Lomolomo anaposema nzi wa kijani kibichi, kwani hao ni nzi wanaokaa sana chooni na kwenye uchafu.
WAHUSIKA
Mama Ntilie
- Ni mama mzazi wa Peter na Zita
- Ni mke wa Mzee Lomolomo
- Mlezi mzuri wa familia
- Ni mvumilivu sana
- Ana huruma
- Ni mchapakazi na anayejituma
- Ana hali ngumu kimaisha
Mzee Lomolomo
- Ni mme wa mama ntilie
- Baba wa Peter na Zita
- Mlevi
- Mvivu
- Si mlezi bora hajali familia
- Anakufa kwa sababu ya kunywa sana pombe
Peter
- Mtoto wa mama ntilie
- Anakosa elimu kwa sababu ya umaskini
- Ana bidii na mchapakazi
- Ana huruma
- Anafungwa jela sababu ya kufanya biashara haramu ya madawa ya kulevya
Zita
- Mtoto wa kike wa mama ntilie
- Anakosa elimu sababu ya umaskini
- Ni mchapakazi
- Anagombana na Kurwa hakupenda aje kwao, roho mbaya
- Anakufa kwa ugonjwa wa kichaa cha mbwa
Doto
- Ni mtoto yatima
- Mtoto wa mtaani
- Doto anauawa baada ya kujiingiza katika uhalifu wa wizi
- Ni mgomvi na katili
Kurwa
- Ni ndugu yake Doto
- Anaishi mtaani
- Ni yatima
- Ana huruma
- Ana nguvu na jasiri
- Ni mchapakazi
- Anaishia jela kwa sababu ya makosa ya Musa na Peter
Zenabu
- Ni jirani wa Mama ntilie
- Ana huruma
- Mfanyakazi wa baa
- Alimsaidia kurwa kumpeleka hospitali baada ya kupandwa na kichaa.
Musa
- Ni mtoto aliyekosa elimu baada ya kukosa sare na ada
- Alikosa malezi mazuri ya wazazi
- Mhalifu, anafanya biashara haramu za madawa ya kulevya
- Ana tamaa ya pesa
- Ni rafiki mbaya kwani alimshauri Peter kuuza madawa ya kulevya
Mwalimu Chikoya
- Ni mwalimu wa akina Peter na Zita
- Aliwafukuza Peter na Zita shule sababu ya kukosa ada
- Si mwalimu mzuri
MANDHARI
Mandhari iliyotumika katika riwaya hii ni mandhari ya jiji la Dar es Salaam. Hii ni kutokana na kutajwa kwa maeneo ya jiji mfano, Manzese, Tabata, Kiwanda cha Urafiki, Kisutu, Muhimbili nk. Pia ametumia mandhari ya nyumbani mfano nyumbani kwa Mama Ntilie uk.5, mandhari ya hospitali ya Muhimbili uk.89, mandhari ya jaani-jaa la Tabata uk.20.
Kwa hiyo mwandishi ametumia mandhari inayosadifu aliyoyaeleza anaibua dhamira halisi zinazosawiri maisha ya Mtanzania wa leo kwa mandhari hiyo mfano suala la umaskini na wimbi la watoto wa mitaani.
0 Maoni