Ad Code

FANI:KILIO CHETU

KILIO CHETU image
Fani: KILIO CHETU
Kilio chetu ni tamthiliya ambayo imejieleza vyema katika fani na maudhui. Tamthiliya hii inamuhusu mhusika Suzi na Joti ambao ni watoto wadogo sana. Wanajiingiza katika mapenzi katika umri mdogo kutokana na ukosefu wa elimu ya kijinsia.
MWANDISHI: MEDICAL AID FOUNDATION
WACHAPISHAJI: TANZANIA PUBLISHING HOUSE (TPH)
MWAKA: 1996

JINA LA KITABU
KILIO CHETU ni jina ambalo linaasadifu yaliyomo katika kitabu. Masuala yanayotajwa mule kama vile upotofu wa maadili kwa vijana wadogo kama Suzi na Joti, suala la mimba za utotoni, madhara ya gonjwa hatari la UKIMWI kwa jamii kweli  ni  kilio chetu ni kilio cha Taifa zima. Kwani katika mambo yanayoiyumbisha jamii kimaendeleo ni upotovu wa maaadili.
Jina hili ni sadifu katika jamii. Mwandishi amelitumia wakati muafaka kabisa kwani mambo anayoyaeleza ndio changamoto katika jamii ya leo. Hivyo kupitia hili jamii si budi kubadilika.

UTANGULIZI WA KITABU
Kilio chetu ni tamthiliya ambayo imejieleza vyema katika fani na maudhui. Tamthiliya hii inamuhusu mhusika Suzi na Joti ambao ni watoto wadogo sana. Wanajiingiza katika mapenzi katika umri mdogo kutokana na ukosefu wa elimu ya kijinsia. Inatueleza kuhusu athari za ugonjwa huu usiobagua. Pia tunafahamishwa kuhusu mtazamo wa wazazi na walezi kuhusu utoaji wa elimu ya jinsia kwa vijana wao. Wapo wanaolipokea kwa mtazamo chanya na wengine hasi.
Kwa ujumla ni tamthiliya nzuri kwani ina mtazamo wa kimabadiliko unaolenga kuwakomboa vijana wetu kutoka katika janga la ugonjwa hatari wa UKIMWI.

FANI

MUUNDO
Tamthiliya ya kilio chetu imefuata muundo wa moja kwa moja au msago. Matukio yameelezwa toka mwanzo mpaka mwisho bila kuruka. Visa na matukio vimegawanywa katika sehemu sita.

Sehemu ya kwanza
Inaonesha jinsi  gonjwa la UKIMWI linavyoikumba jamii. Mwandishi anaeleza kuhusu Dubwana linaloikumba jamii.

Sehemu ya pili
Mwandishi anaeleza kuhusu athari za UKIMWI, jambo ambalo lilipelekea kifo cha Fausta. Pia Suzi agundulika kujihusisha na mapenzi baada ya kukutwa na vidonge vya kuzuia mimba.

Sehemu ya tatu
Inaeleza juu ya watoto ambao wameshajiingiza katika suala la mapenzi licha ya kuwa na umri mdogo mfano ni Joti na Suzi. Pia madhara ya utandawazi yanaelezwa hapa mfano kuoneshwa kwa picha za ngono.

Sehemu ya nne
Tunaelezwa juu ya tabia hatarishi za Joti za kuwa na mahusiano na wasichana wengi mfano Chausiku, Yoranda, Gelda na Suzi. Hapa Joti anafanikiwa kumrubuni tena Suzi. Pia tunaoneshwa jinsi Ana anavopingana na vishawishi kutokana na kupata elimu ya jinsia.

Sehemu ya tano
Suzi anagundulika kuwa na mimba ya Joti, anajutia kosa hilo anajilaumu sana.

Sehemu ya sita
Inatuonesha jinsi Joti alivyokuwa magonjwa tayari kutokana na UKIMWI. Hapa ushauri mzuri unatolewa kuhusu namna ya kumtunza mgonjwa wa UKIMWI na kumfanya aishi kwa matumaini. Hapa mwandishi anapinga mila potofu kuhusu UKIMWI kuwa si kurogwa bali ni ugonjwa unaoambukizwa.

MTINDO
Tamthiliya hii imesheheni katika mitindo kadha wa kadha inayopamba kazi hii. Mtindo uliotumika ni dayalojia au majibizano.
Mwandishi ametumia mtindo wa mianzo na miisho ya kifomula ya usimulizi ambao ni mtindo wa usimulizi wa fasihi ya kiafrika. Mfano uk.1 mwandishi anasema “paukwa….. pakawaa…. Niendelee…. nisiendelee? ….. au mmechoka? Uk.113, pia uk.36 mwandishi anasema “na hadithi yangu imeishia hapo”. Pia mwandishi ametumia mtindo wa utambaji kwani ndiye anayesimulia na kuelezea matukio.

Matumizi ya nafsi
Nafsi ya pili ndiyo iliyotawala, mwandishi ametumia majibizano ya watu wawili mfano Suzi na Joti, pia watu watatu n.k.
Pia mwandishi ametumia tanzu nyingine za fasihi mfano wimbo uk.27

WAHUSIKA
SUZI
  • Ni binti mdogo wa darasa la sita
  • Anajihusisha na mapenzi na Joti
  • Hana msimamo
  • Anapata mimba katika umri mdogo
  • Ana hatari ya kuwa na UKIMWI
  • Hakupewa elimu ya jinsia
  • Ana tamaa kwani alitamani vitu alivyohongwa na Joti.

JOTI
  • Ni kijana mdogo wa kiume
  • Ana mahusianao ya mapenzi na wasichana wengi Suzi, Gelda, Yoranda na Chausiku
  • Hana elimu ya jinsia
  • Ana makundi mabaya ya marafiki
  • Anaathirika na kufa kwa gonjwa la UKIMWI
  • Amechangia kuharibu maisha ya Suzi kwa kumrubuni
  • Ni mlaghai
  • Hafai kuigwa na jamii

MAMA SUZI
  • Ni mzazi wa Suzi
  • Anashikilia ukale hataki mabadiliko
  • Hampi mwanae elimu ya jinsia
  • Alichangia kuharibu maisha ya Suzi
  • Ni mkali sana katika malezi hatumii busara bali hasira
  • Hafai kuigwa na jamii
BABA JOTI
  • Ni mzazi wa Joti
  • Hayupo tayari kutoa elimua ya jinsia
  • Anashikilia ukale
  • Ni mkali anatumia viboko kuelimisha jambo ambalo si sahihi
  • Amechangia kuharibu maisha ya Joti
  • Ni muhuni, si muaminifu katika ndoa yake
  • Hafai kuigwa na jamii

ANNA
  • Ni binti mdogo wa shule
  • Ana elimu ya jinsia
  • Ana msimamo mzuri anashinda vishawishi
  • Anatoa elimu kwa vijana wenzake kuhusu athari za kujiingiza katika mapenzi katika umri mdogo
  • Ana tabia njema
  • Hana tama
  • Anafaa kuigwa na jamii

BABA ANNA
  • Ni mzazi wa Anna
  • Anatoa elimu ya jinsia kwa wazazi na watoto
  • Ni mlezi bora
  • Alichangia maisha ya Anna kuwa ya mafanikio
  • Anafaa kuigwa na jamii

MJOMBA
  • Ni kaka yake Mama Suzi
  • Anaendana na wakati wa sasa
  • Anatoa elimu ya jinsia kwa vijana na wazazi
  • Ni mlezi bora ni mshauri bora
  • Anatoa elimu ya UKIMWI kwa Baba Joti anapinga mila potofu
  • Anafaa kuigwa na jamii
MAMA JOTI
  • Mzazi wa Joti
  • Ndoa yake ipo matatani kuingiliwa na mke mwingine
  • Anaelewa kuwa jamii imebadilika na wazazi wanapaswa kuwaelimisha watoto

JIRANI
  • Ni jirani wa Baba Joti
  • Ana imani potofu za kishirikina, anaamini Joti alilogwa
  • Haamini kuwa UKIMWI upo

CHAUSIKU
  • Ni msichana wa mtaani
  • Mfanyabiashara wa vitumbua
  • Ni jirani wa Suzi
  • Ana tabia mbaya ni muhuni
  • Alichangia kuharibu maisha ya Joti
  • Ana mahusiano ya kimpenzi na vijana wadogo mfano Joti na watu wazima pia, mfano Mpemba

CHOGO, MWARAMI NA JUMBE
  • Ni marafiki wa Joti
  • Ni wanafunzi wadogo
  • Si marafiki wazuri
  • Wana tabia mbaya wanashauriana kuhusu mambo mabaya
  • Hawafai kuigwa na jamii

MANDHARI
Mandhari aliyoitumia mwandishi ni ya mjini, hii ni kutokana na maelezo ya mhusika jirani anaposemauk.32 “……mie toka siku ile nimwone hospitali sijakaa mjini. Nilikwenda zangu shamba kupambana na Nyani wala nafaka.” Pia lugha ya mtaani iliyotumiwa na vijana Joti, Mwarami na wenzake, masuala ya picha ya “X” yaani viashiria vya mambo ya mjini kwani yamekithiri sana mijini. Maeneo yanayotajwa kama vile uwanja wa Sabasaba ni uwanja uliopo mjini, masuala ya lifti kwa wasichana hasa wanafunzi yapo mijini. Mfano.uk.27 pia kuna mandhari ya nyumbani na mtaani.
Mandhari aliyotumia mwandishi inasawiri maudhui yake katika jamii.  Kwani anaibua mambo yaliyo katika jamii.

MATUMZI YA LUGHA
Lugha iliyotumika ni lugha iliyo na ubunifu wa kipekee wenye mvuto wa kisanaa. Lugha ni rahisi na inayoeleweka vyema kwa hadhira lengwa. Pia kuna matumizi ya lugha nyingine mfano kiingereza na lugha za kikabila. Kiingereza mfano uk.21 “tuition” uk.16 “come”. Lugha za kikabila mfano wimbo uk.35
                                               “Joti afitwe sanda salauya
                                                  Ena ena salauya            
                                                   …………………….”
  • Matumizi ya lugha ya mtaani.
Mfano uk.16 “mshefa” “mshikaji”-rafiki.
Uk.17 “kamba” – kudanganya jambo
Uk.22 “vidosho” – wasichana
Uk.16 “kanitolea nje” – kukataa jambo fulani.

  • Matumizi ya tamathali za semi.

Tashibiha
Uk.1 “wakapukutika kama majani”
Uk.5 “mgumu kama mpingo”
Uk.6 “miti inaungua kama mabua”
Uk.13 “Dubwana limetanda kama utando wa Buibui”

Tashihisi
Uk.2 “vifo vikawazoa” kifo huua tu lakini kimepewa uwezo wa kuzoa

Sitiari
Uk.8 “We Mbwa mweusi”
Uk.9 “Nyoka wee”
Uk.21 “huyo kinyago wako anakimbia nini?”

Tafsida
Uk.4 “kafa kwa kukanyaga nyaya” – kafa kwa UKIMWI

Mubaalagha
Uk.4 “Mtu si mtu, kizuka si kizuka”
               
  • Matumizi ya mbinu nyingine za kisanaa.

Tanakali sauti/ Onomatopea
Uk. Joti akasema “….acha moyo unipwite “Pwi! Pwi! Pwi!”
Uk.25 “….hebu nitolee uchafu wako mie ptuu!”

Tashtiti
Uk.15 “….huyu ni Suzi kweli au nani?”
Uk.36 “kwanini Joti……… kwanini Joti afe?”
                                    
Takriri
Uk.1 “watu wakapukutika, wakapukutika…..” “tunakwisha, tunakwisha”
Uk.2 “vifo vikawzoa, vikawazoa .…. vikawazoa”
Uk.16 “piga domo, piga domo”

  • Matumizi ya semi

Methali
Uk.6 “wembamba wa Reli Treni inapita”
Uk.11 “mzazi usipomfunza walimwengu watamfundisha”
Uk.19 “shukrani ya Punda ni mateke”
Uk.24 ‘Ndege mjanja ananaswa na tundu bovu

Nahau
Uk.6 “nimekuvulia kofia”- nakuheshimu
Uk.21 “anajigongagonga” – anajipendekeza

Misemo
Uk.4 “kuwa nyumanyuma kama koti”
Uk.6 “kifua simkingii maana siwi naye”
Uk.7 “makapera kibao Mume wangu wa nini?”
Uk.22 “mapenzi ni tiba”
Uk.26 “…..unakimbilia suti na nepi hujavaa”

  • Matumizi ya taswira.
uk.1 “dubwana” – ugonjwa wa UKIMWI
Uk.7 “Nguru” – aina ya Samaki wabaya – amefananishwa na mtu mbaya
Uk.21 “kinyago” - Suzi

Chapisha Maoni

0 Maoni